SOMO: UMUHIMU WA KUJISOMEA MWENYEWE ILI USIDANGANYWE

 SOMO: UMUHIMU WA KUJISOMEA MWENYEWE ILI USIDANGANYWE


Katika dunia ya sasa, watu wengi wamepoteza tabia ya kujisomea wenyewe. Badala yake, wamekuwa wakitegemea kusikia na kuona tu kutoka kwa wengine—kupokea taarifa bila kuchunguza ukweli wake. Hali hii imewafanya wengi kudanganywa kwa urahisi, kufuata upotoshaji wa kweli bila hata kugundua.


Katika Danieli 9:2 tunajifunza jambo la msingi sana:


"Katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danielii, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini."


Danieli hakusubiri kusimuliwa na watu wengine kuhusu ahadi ya Mungu. Alijisomea mwenyewe maandiko ya nabii Yeremia, akachunguza na akaelewa mpango wa Mungu kuhusu miaka sabini ya ukiwa wa Yerusalemu. Kwa kusoma mwenyewe, Danieli alipata maarifa sahihi na akajua nini kilikuwa kitatokea.


Hili linafundisha nini?

Kama Danieli angekuwa tegemezi wa kusikia tu, asingelifahamu kwa usahihi mpango wa Mungu kwa watu wake. Lakini kwa kusoma vitabu, alifahamu maamuzi ya Mungu na akajiandaa kwa maombi (Danieli 9:3).


Maandiko mengine yanayotuonya kuhusu kutokujisomea:


Hosea 4:6


"Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umekataa maarifa, mimi nami nitakukataa, usiwe kuhani kwangu..."

Watu wanapopuuza maarifa ya kweli kwa kukosa kujisomea, wanajiweka katika hatari ya kupotea na kupotoshwa.


Matendo ya Mitume 17:11


"Watu hawa walikuwa waungwana zaidi kuliko wale wa Thesalonike; kwa maana walilipokea lile neno kwa usikivu mkuu, wakayachunguza maandiko kila siku, ili waone kama mambo hayo yalivyo."


Waeberea walikuwa waungwana kwa sababu hawakuridhika tu na walichosikia; walichunguza maandiko kila siku ili kujihakikishia ukweli. Hii ndiyo roho ambayo tunapaswa kuwa nayo.


1 Yohana 4:1


"Wapenzi, msiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wametokea duniani."


Tunaamriwa kuchunguza, kujaribu na kuthibitisha kabla ya kuamini. Hii haiwezekani kama hatujijengei tabia ya kujisomea.


MATOKEO YA KUTOKUJISOMEA:


Kudanganywa na mafundisho ya uongo.


Kuangukia hofu na propaganda za dunia.


Kupoteza nafasi ya kupokea maarifa ya Mungu.


Kuishi maisha bila msingi wa kweli.


HITIMISHO:


Leo hii, tusikubali tu kusikia na kuona bila kuchunguza. Jifunze kujisomea mwenyewe. Fungua vitabu vya Mungu, chunguza, tafakari, na fahamu ukweli. Kama Danieli, tupate kuelewa mapenzi ya Mungu kupitia kujituma katika kujifunza. Hii ndiyo njia ya pekee ya kulinda imani na maisha yetu dhidi ya udanganyifu wa ulimwengu huu.


"Jitahidi kujionyesha kuwa umefaulu mbele za Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukilitumia vema neno la kweli."

(2 Timotheo 2:15)


Imeandaliwa na:

Kisakenyi Mnzava

Mwalimu wa Neno la Mungu na Mshauri wa Mahusiano

WhatsApp: 0764 317 590

Barua pepe: issacklucas2@gmail.com

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

KWANINI WATU WENGI LEO WANAABUDU WATU NA SIO MUNGU?

📖 HAKUNA MWANADAMU MKAMILIFU

KWANINI NIOGOPE SIKU ZA UOVU?